Tuesday 11 August 2015

Achomwa na pasi ya umeme sehemu mbalimbali mwilini na dada yake, kisha kufungiwa ndani kwa siku tatu mfululizo.

Mtoto wa miaka 11 anayesoma Shule ya Msingi Shauri Moyo mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kuchomwa na pasi ya umeme sehemu mbalimbali mwilini na dada yake, kisha kufungiwa ndani kwa siku tatu mfululizo.
Akizungumza kwenye ofisi za Mwananchi, mtoto huyo (11),  anayesoma darasa la sita alidai kuwa ukatili huo amefanyiwa na dada yake wanayechangia baba.
Alidai kuwa Agosti 6 baada ya kurudi kutoka shule, dada yake alimtuhumu kumuibia Sh30,000 na mafuta ya kupaka.
“Nilimweleza kwamba sihusiki na wizi huo, lakini yeye hakukubali alichukua pasi na kuanza kunichoma nayo kwenye mapaja, mgongoni na kifuani,” alisema mtoto huyo.

Mtoto huyo anadai kuwa, baba yake aliporudi alimweleza kuwa amechomwa moto, lakini cha kushangaza alijibiwa kuwa aache kwenda kwa watu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Shaurimoyo, Felix Ngowi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema yeye kama kiongozi wa mtaa amepinga ombi la baba mzazi wa mtoto huyo kutaka suala hilo kumaliza kifamilia.
“Tulipata taarifa na polisi walifika na kuwakamata watuhumiwa na kumpeleka mtoto hospitalini ambako anaendelea vizuri,” alisema.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Fulgens Ngonyani amekiri kupokea taarifa za ukatili huo na kusema tayari linawashikilia watuhumiwa wote wawili na uchunguzi ukikamilika watafikishwa kortini.

0 comments:

Post a Comment