Friday 26 February 2016

Ester Bulaya Atamba 'Nitaendelea Kumgaragaza Wasira Ubunge wangu si Wakuchakachua'


Mbunge wa Bunda Mjini, mkoani Mara, Esther Bulaya (Chadema), ametamba kuwa ataendelea kumshinda mpinzani wake kisiasa, Stephen Wasira (CCM), kwa madai kwamba alipata ubunge huo kihalali.

Bulaya alisema hayo jana ikiwa ni siku moja tangu kutupwa kwa rufaa ya wanachama wa CCM waliokuwa wakipinga ushindi wa mbunge huyo alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 dhidi ya Wassira na wagombea wa vyama vingine.

Mbunge huyo aliiambia Nipashe kwa njia ya simu kutoka jimboni kwake kuwa, alimshinda Wasira kwa wananchi, akamshinda kisheria, lakini hakuridhika akakata rufaa na ameendelea kumshinda.

"Kama ana mpango wa kukata rufaa nyingine aende akate tu, lakini akumbuke kuwa nitaendelea kumshinda tu kwa sababu ubunge wangu sio wa kuchakachua bali nimeupata kutokana na kura za wananchi wa Bunda Mjini," alisema Bulaya na kuongeza:

"Siku zote nimekuwa nikisema kuwa waliofungua kesi sio wanachama wa CCM bali ni Wasira mwenyewe, ndio maana akawa mkali kupigwa picha na waandishi ili Watanzania waendelee kudhani kwamba hayumo katika kesi hiyo," alisema.

Alisema wakati umefika sasa mwana siasa huyo mkongwe kupumzika na kula mafao yake, kwa kile alichosema ametumikia taifa kwa muda mrefu na sasa ni zamu ya wengine kumpokea kijiti ili kuanzia pale alipoachia.

"Pamoja na hayo ninamkumbusha kuwa siku zote mahakama husimamia haki ndio maana ameshindwa mara mbili katika kesi hii, hivyo hana budi kupumzika," alisema.

Januari 25 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilitupilia mbali kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa na wapigakura Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagira kupinga ubunge wa Bulaya.

Bulaya alihama CCM na kujiunga na Chadema katikati ya mwaka jana na kuteuliwa na Chadema kuwania ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini na kufanikiwa kumbwaga mkongwe huyo kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana

0 comments:

Post a Comment