Monday 8 February 2016

Mnyonge Mnyongeni Rais Magufuli Ndio Rais Tuliyokuwa Tunamtaka Tanzania...Ukweli Utabaki pale pale

Mungu ni mwema hatuna budi kumshukuru kwa anayotufanyia
katika nchi yetu.
Baada ya kusema hayo niseme bila kumung’unya maneno
kwamba Rais Dk. John Pombe Magufuli ndiye rais tuliyekuwa
tunamtaka kutokana na anachokifanya sasa.
Nichukue nafasi hii kumpongeza kwa hatua anazochukua ili
kuwafanya wananchi wanufaike na rasilimali za nchi hii, hivyo
namtakia kila la heri katika kazi yake ya kututumikia. Naomba
kukiri kwa uwazi kwamba Watanzania tulifanya chaguo sahihi,
hatukukosea.
Tanzania ina vyama 23 vya siasa vilivyosajiliwa na
vinavyofanya kazi sasa, tutake tusitake Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kilimuona Dk. Magufuli kuwa ni tunu ya taifa na leo
anadhihirisha hilo kwa kupigania wananchi wake na kuwa adui
kwa mafisadi.
Kila Mtanzania sasa anaamini kwamba Dk.Magufuli anaweza
kurejesha bila wasiwasi usimamizi thabiti wa serikali na
nidhamu ya utendaji ndani ya serikali. Naamini kuwa serikali
ya Magufuli itakuwa ya kiusimamizi na yeye mwenyewe
anaweza kulifanya jambo hilo bila kusita. Tumeona.
Katika nyadhifa nyingi alizopitia hadi sasa ameijenga taswira
hii kila alikopita na bado inambeba katika awamu hii ya
tano.Hakuna siri, kama kuna jambo ambalo lilikuwa haliendi
sawa nchini ni la utendaji ndani ya serikali. Tunafahamu kuwa
wafanyakazi ndani ya serikali ukiachilia mbali matatizo
waliyonayo kwa maana ya vipato, hata mambo madogo
ambayo wangeweza kuyasimamia ndani ya dakika au saa
chache yalichukua wiki hata miezi kadhaa.
Utaratibu wa utoaji huduma ulikwama sana lakini kwa spidi ya
Rais Magufuli atafanikiwa kutatua changamoto hiyo kubwa na
ya siku nyingi. Ikiwa utendaji wa serikali unaimarika na
huduma zinatolewa kwa wakati, tutaweza kujenga taifa
linalokwenda mbele kimaendeleo.
Taswira bora ya pili ya serikali ya Dk. Magufuli ni misimamo
katika masuala ya msingi na kutoyumba. Magufuli muda wote
ambao amekuwa kiongozi anaonesha njia, ndiyo maana
alipoanza tu kazi, alianza na tabia ya ziara za kushtukiza. Hii
alikuwa akifanya hata alipokuwa waziri wa ujenzi.
Moja ya mambo ambayo serikali iliyopita ilikosa ni pamoja na
kukosa misimamo na kuwa na Double standard. Mfano
mdogo tu ni kwenye mchakato wa Katiba Mpya ambapo rais
anayeondoka alisimamia uanzishwaji bora wa mchakato huo,
akaunga mkono katika hatua zote na rasimu zote, lakini akaja
kuwageuka wajumbe wa tume hiyo na rasimu yao ya pili
alipolihutubia Bunge Maalumu la Katiba.
Naamini Magufuli si mtu wa kugeuka na kuna masuala mengi
anaweza kuyasimamia kwa dhati na kila mmoja wetu
akakubali kuwa, huyu ni kiongozi anayesimamia haki na ana
uchungu na wananchi wake.
Amekuwa akitetea wanyonge hadharani mara nyingi na
anaonekana wazi kwamba anaumizwa na watu wanaoibia
serikali bila kujali kuwa kuna watu wanakosa mlo mmoja kwa
siku.
Wote tumuunge mkono, ni rais anayestahili sifa hizo,
mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kwa kufanya
hivyo naamini tutashinda.
Jipu limepasuka siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.


0 comments:

Post a Comment