Thursday 18 February 2016

Kambi ya Upinzani bungeni Yaendelea Kumgomea Spika Ndugai

Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu
amesema kambi hiyo haitaongoza kamati za Bunge za Hesabu
za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) hadi
ofisi ya Spika itakapobadilisha uteuzi wa wajumbe wa kamati
hizo.
Kwa mujibu wa mabunge ya Jumuiya za Madola, kamati hizo
huongozwa na wapinzani, lakini tangu Spika wa Bunge, Job
Ndugai afanye uteuzi wa wajumbe, kambi hiyo imesusia
kushiriki uchaguzi kwa kile wanachokiita “kupangiwa
wajumbe”.
Jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema
mazungumzo kati ya ofisi ya spika na kambi hiyo bado
yanaendelea na kusisitiza kwamba uteuzi huo unaweza
kutenguliwa au kuachwa kama ulivyo.
Katika maelezo yake, Lissu alisema licha ya kambi hiyo kuwa
katika mazungumzo na ofisi ya spika, suluhisho
halijapatikana na kusisitiza kuwa msimamo wao upo
palepale.
“Hatujafika popote. Msimamo wetu uko palepale na
hatutakubali kuchaguliwa viongozi wa hizo kamati na CCM,
kama wanafikiria ni lazima iwe wanavyotaka sisi
hatutakubali,” alisema.
Joel aliwahi kunukuliwa na na vyombo vya habari akisema
kuwa kama kambi hiyo itasusia uchaguzi, shughuli za kamati
zitafanywa na makamu wenyeviti ambao wanatokea CCM.
“Ni bora tusiziongoze kabisa kamati hizi. Ukifuatilia utabaini
kuwa katika PAC na Laac tuna wajumbe sita kila kamati kati
ya wajumbe 23, wakati huohuo kamati ya Ukimwi tumepewa
wajumbe 12 kati ya wote 23,” alisema Lissu.
Alisema wajumbe sita waliopo katika kamati ya Laac na PAC
wameteuliwa na CCM na kama kamati hizo zinaongozwa na
upinzani ni lazima wapinzani wajichagulie wajumbe wao,
wakiwamo watakaochaguliwa kuwa wenyeviti. Alisema wabunge
wana haki sawa, lakini hawana uwezo sawa.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), alisema uamuzi wa spika kuwapangia wajumbe
katika kamati hizo hauna nia nzuri na kwamba, huenda ni
mkakati wa ofisi hiyo kuifanya Serikali iwe inapitisha mambo
yasiyofaa bungeni.
Februari Mosi mwaka huu, Kambi ya Upinzani bungeni ilisusia
uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo kwa maelezo kuwa Spika
Ndugai alifanya uteuzi ‘kiholela’ na kuahidi kutoshiriki
mpaka pale watakapopewa idhini ya kupendekeza wenyeviti.



0 comments:

Post a Comment