Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

Friday, 26 February 2016

Majina Ya Mawaziri MAJIPU Yakabidhiwa Kwa Waziri Mkuu......Ni Wale Waliogoma Kutangaza Mali Zao

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa majina ya baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri ambao hawajajaza fomu za mali wanazozimiliki kama sheria inavyowataka.

Akizungumza jana kwenye semina ya mawaziri na naibu mawaziri, Kamishina wa Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema viongozi hao wanajua umuhimu wake lakini wanapuuza.

“Sheria hii ya Maadili ya Viongozi wa Umma inajulikana, lakini jambo la kushangaza wapo baadhi ya mawaziri na manaibu ambao hawajajaza, kwa ruhusa yako nitakukabidhi majina yao, sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, hivyo anayekiuka anapaswa kuadhibiwa,” alisema Jaji Kaganda bila kutaja majina hayo.

Kifungu cha 9 cha sheria hiyo kinataka katika kipindi cha siku 30 baada ya kupewa wadhifa, kila mwisho wa mwaka na mwisho wa kutumikia wadhifa wake kiongozi husika anatakiwa kupeleka tamko la maandishi la mali zake.

Sheria hiyo inafafanua kuwa mali hizo ni pamoja na rasilimali zake au mume au watoto wenye umri usiozidi miaka 18 ambao hawajaoa au kuolewa.

Alisema fomu hizo lazima zijazwe na viongozi na wananchi wanaruhusiwa kwenda kuzihakiki wakitoa sababu za msingi, lakini sheria hiyo hairuhusu waende kutangaza na wakifanya hivyo hatua zinachukuliwa dhidi yao.

“Hapo ndipo wananchi wengi huwa hawatuelewi kwa kuwa wanapenda kujua mali ambazo viongozi wao wanamiliki,” alisema.

Alisema Sekretarieti kwa kutambua umuhimu wa viongozi hao kuzingatia sheria na maadili, ndiyo sababu imeandaa semina hiyo baada ya kupata ufadhili kutoka Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID), wakiamini kuwa yatasaidia kuwakumbusha.

Wednesday, 24 February 2016

Mambo Yazidi Kufichuka...Ezekiel Maige Nae Atajwa Ufisadi Ngorongoro

Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii katika serikali
ya awamu ya nne, Ezekiel Maige, jana alitajwa
katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bernard
Murunya ambaye ameshitakiwa kwa matumizi
mabaya ya ofisi.
Katika kesi hiyo, Maige anadaiwa kulipiwa nauli ya
safari ya nje na mamlaka hiyo kwa idhini ya
Murunya, ambaye sasa ni Mbunge wa Afrika
Mashariki.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Sezari Semfukwe,
alidai kuwa Murunya na aliyekuwa Mkurugenzi wa
Fedha na Utawala wa Mamlaka hiyo, Shad Kiambile,
waliidhinisha malipo ya dola 66,890. Alidai kuwa
fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya safari ya Maige na
msaidizi wake aliyetajwa kwa jina la E. Muyungi na
Murunya mwenyewe.
Semfukwe, ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa
mamlaka hiyo, alidai kuwa Murunya na Kiambile,
ndio walioidhinisha madokezo kwa ajili ya malipo
hayo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Hamidu Sembano,
akisaidiana na Rehema Mteta, mbele ya Hakimu wa
Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda,
Semfukwe alidai kuwa utaratibu wa maombi ya
safari, unatokana na maelekezo ya mkuu wa idara
na kujaza fomu inayoonyesha anakwenda wapi na
kwa muda gani.
Sambamba na hilo, alidai kuwa aina zingine za safari
zinahusisha watu wa nje ambao, si waajiriwa wa
NCAA kwa dokezo la mkuu wa idara au shirika.
Alidai kuwa alitoa hundi ya malipo namba 309/0238
ya Septemba 9/2011, ambayo ilikuwa na dokezo la
safari kutoka kwa Murunya kwenda kwa Mkuu wa
Kitengo cha Fedha. Pia alitoa hundi ya malipo
nyingine iliyokuwa ikionyesha imelipwa dola
zaMarekani 66,890 kwa kampuni ya Wakala wa
Usafirishaji ya Cosmas.
Aliendelea kudai kuwa hundi za malipo namba
310/0379 ya Oktoba 29, 2011 na ankara namba 5609
ya Septemba 7,  2011 zililipwa kwa Antelope Tours &
Traveling kwa ajili ya tiketi za Murunya, Muyungi na
Maige kwa malipo ya dola za Marekani 66,890 (zaidi
ya Sh. milioni 133).
Shahidi hiyo alidai kuwa kumbukumbu ya kitabu cha
malipo ya hundi inaonyesha hundi namba 002758 na
002755 za Septemba 9, 2011 zililipwa kwa kampuni
ya Cosmas Travelling Agent na zilitiwa saini na
Kiambile na Murunya.
Hata hivyo, wakati shahidi huyo akitoa vielelezo hivyo
mahakamani hapo ili vitumike kama ushahidi,
malumbano ya kisheria yaliibuka baina ya mawakili
wa pande zote.
Malumbano hayo yaliibuka baada ya upande wa
washtakiwa, ukiongozwa na wakili Amani Mirambo,
kutaka kujua ni vielelezo vingapi au vya aina gani
ambavyo upande wa mashtaka unavileta.
Hatua hiyo ilisababisha malumbano ya kisheria hivyo
kumfanya hakimu kuahirisha kesi kwa dakika 10.
Baada ya muda huo, alirejea mahakamani baada ya
dakika hizo na kuwahoji.
Baada ya kuhoji pande zote mbili, kutokana na
malumbano ya kisheria, Hakimu alikatizwa na Wakili
wa Serikali Hamidu Simbano, aliyemwomba
kuahirisha kesi hiyo na kutaja tarehe nyingine ya
washtakiwa kusomewa maelezo yao ya awali.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Rehema Mteta,
aliwasomea maelezo ya awali juu ya tuhuma za
matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha
mamlaka hiyo kupoteza dola 66,890 (Sh.
133,780,000).
Mteta aliwataja washitakiwa, mbali na Murunya na
Kiambile, kuwa ni Meneja Utalii wa mamlaka hiyo,
Veronica Funguo na Salha Issa ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Cosmas Travelling Agent.



Monday, 22 February 2016

Profesa Ibrahim Lipumba Aibuka....Amtaka Rais Magufuli Atangaze Mshahara Na Marupurupu Yake

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba amemtaka Rais John Magufuli atangaze
mshahara na marupurupu yake, kwa kuwa
amejivisha joho la kuwa Rais wa wanyonge.
Profesa Lipumba amelieleza gazeti la Mwananchi
kuwa Rais Magufuli amejipambanua kuwa kiongozi
anayeguswa na matatizo ya wanyonge, hapendi
makuu, anahimiza ukusanyaji wa mapato ya Serikali
na matumizi mazuri ya fedha za umma, lakini
watanzania hawajui mshahara wake ni kiasi gani
Profesa huyo aliyejikita katika masuala ya uchumi,
alirejea mijadala mbalimbali iliyowahi kuibuliwa
kuhusu mshahara wa Rais, ikiwamo ule uliyowahi
kuibuliwa mwaka 2013 na Zitto Kabwe, wakati huo
akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kuwa Rais
analipwa Sh32 milioni kwa mwezi.
Pia alirejea taarifa iliyochapishwa na Mwananchi,
Julai 27, 2015, iliyoandikwa kutoka katika mtandao
wa African Review kuwa Rais mstaafu Jakaya
Kikwete ni wa nne miongoni mwa marais wa Afrika
kwa kupata mshahara mkubwa wa dola za Marekani
192,000 kwa mwaka sawa na dola 16,000 kwa mwezi,
ambayo ni sawa na Sh32 milioni kwa mwezi. Hadi
jana jioni, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na
Sh2,187.
“Taarifa ya Ikulu ilikanusha vikali habari
zilizochapishwa na Mwananchi. Ikulu ilieleza kuwa
habari hizo siyo za kweli. Hata hivyo, haikueleza
mshahara wa Rais na marupurupu yake ni kiasi
gani?
Pia, katika mjadala wa mshahara wa Rais, Naibu
Spika wa Bunge lililopita ambaye ndiye Spika wa sasa,
Job Ndugai alinukuliwa akieleza kuwa mshahara wa
mtu ni siri yake.
Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
utumishi wa Umma wa wakati huo, Celina Kombani
(kwa sasa ni marehemu) alisema kuwa ni kosa
kutangaza mshahara wa Rais.
“…Kwa hivi sasa Rais Magufuli atangaze mshahara
na marupurupu yake na kama mapato yake ni Sh32
milioni kwa mwezi, basi ajitolee alau nusu ya mapato
hayo kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Hatua
hii itaimarisha taswira inayojengeka barani Afrika
kuwa yeye ni Rais wa wanyonge,” amesema Lipumba.
Wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam wiki
iliyopita, Rais Magufuli aliwataka mawaziri, naibu
mawaziri na makatibu wakuu wachangie Sh1 milioni
katika mishahara yao kuchangia elimu.
Pia Rais alieleza kuwa yeye mwenyewe, makamu wake
na waziri mkuu watachangia Sh6 milioni kila mmoja,
ili zifike Sh100 milioni kusaidia changamoto za elimu
bure Mkoa wa Dar es Salaam.
Kutokana na tangazo hilo, Profesa Lipumba alisema,
“Ikiwa Sh6 milioni zitakatwa katika mshahara wake
wa mwezi mmoja ni wazi mshahara wake na ule wa
makamu wake na waziri mkuu ni zaidi ya Sh6 milioni
kwa mwezi.
“Mishahara na marupurupu ya viongozi wa Tanzania
hayako wazi. Watanzania hawajui kila mwezi Rais,
Makamu wa Rais na viongozi wakuu wa Serikali
wanalipwa kiasi gani? Malipo ya wabunge pia hayako
wazi?” alihoji.
Profesa Lipumba ambaye amewahi kuwa msaidizi wa
Rais katika masuala ya uchumi kati ya mwaka 1991
na 1993, alisema kwa kuwa Rais Magufuli amejivisha
joho la kuwa Rais wa wanyonge, anawajibika
kuwaeleza Watanzania mshahara na marupurupu
yake.
“Ikiwa mshahara ni mkubwa sana achukue hatua za
kuupunguza kama alivyofanya Mwalimu Nyerere
mwaka 1965.”
Hata hivyo, alisema kifungu cha Katiba cha 43 (2)
kinaeleza kuwa mshahara na malipo mengineyo yote
ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa
bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa
masharti ya Katiba.
Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli akitaka
kupunguza mshahara wake itabidi kwanza abadilishe
kifungu hicho cha Katiba.
“Anaweza kujitolea mchango wa kudumu
utakaokatwa kutoka kwenye mshahara wake
kusaidia sekta ya afya au elimu,”alisema.
Profesa Lipumba ambaye ni mshauri wa Benki ya
Dunia (WB) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika
masuala ya uchumi, alisema ili kuimarisha utawala
bora ni muhimu uongozi ulio madarakani utumie
mamlaka waliopewa kwa manufaa ya Taifa.
“Mishahara na marupurupu ya viongozi yawe wazi na
yaamuliwe na kupangwa na taasisi iliyo huru. Kuweka
utaratibu ulio wazi wa kuamua mishahara na
marupurupu ya viongozi wa umma wakiwamo Rais na
makamu wake, mawaziri, wabunge, majaji, makatibu
wakuu na viongozi wengine,”alisema.
Alisema ni muhimu katika ujenzi wa utawala bora,
uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa umma kwa
wananchi wanao waongoza.
“ Inasemekana mshahara wa mbunge katika Bunge
lililopita ulikuwa Sh3.4 milioni kila mwezi.Pia mbunge
alilipwa Sh8.2 milioni, nyingine kama posho ya jimbo,
gharama za ofisi, mafuta, malipo ya wasaidizi wake
na dereva.
“Vile Vile, mbunge anapohudhuria kikao cha Bunge
alilipwa posho ya Sh80,000 za kujikimu, Sh50,000 za
mafuta ya gari na Sh200,00 za kuhudhuria kikao cha
Bunge, jumla ni Sh330,000 kwa siku.
“Posho ya siku moja ya mbunge ni zaidi ya mara mbili
ya kima cha chini cha mshahara wa Serikali kwa
mwezi mzima ambacho ni Sh150,000. Mishahara
inakatwa kodi, marupurupu hayakatwi kodi,”alisema.


Magufuli Alivyotinga Kivukoni na Magari Yenye Namba za Kawaida Bila Taarifa..

Rais John Magufuli ameendelea kufanya ziara za
kushtukiza, baada ya kutembelea ofisi za Kivukoni
Dar es Salaam kimyakimya juzi jioni kuangalia
mwenendo wa utoaji huduma za vivuko.
Mashuhuda waliokuwepo eneo hilo Jumapili jioni
wakati Rais anafanya ziara hiyo, walieleza mtindo
alioingia nao Dk Magufuli ulikuwa ni wa kawaida na
vigumu kwa mwananchi wa kawaida kung’amu uwapo
wa Rais.
Mfanyabiashara wa eneo hilo, Sharif Mkamba
alisema Rais Magufuli aliingia saa 11 jioni akiwa na
msafara wa magari matatu ya kawaida yaliyokuwa
na namba za kiraia.
“Hakukuwa na king’ora chochote kama tulivyozoea
bali ulikuwa ni msafara wa kimya kimya. Aliingia
moja kwa moja kwenye zile ofisi na alitumia kati ya
dakika 10 hadi 15 kabla ya kutoka,” alisema
Mkamba.
Said Likoko alisema kuwa baada ya kugundua kati ya
magari matatu alikuwepo Rais, walisogea kufuatilia
kwa kina kwa kuwa haijazoeleka na walitegemea
huenda baadhi ya watumishi wangewajibishwa.
“Aliteremka na kumuuliza aliyemkusudia na taarifa
tulizozipata jana zinadai hakumkuta huyo bosi, sijui
ni meneja au ofisa sisi hatujui,” alisema Likoko
ambaye hujishughulisha pia na biashara ndogondogo
eneo la kivukoni.
Likoko alisema pamoja na kwamba aliingia kimya
kimya, Rais Magufuli hakusita kuwasalimia wasafiri
waliokuwa wakisubiri kivuko wakati alipofanya ziara
hiyo.
Alieleza kuwa kama wananchi walifurahishwa na
hatua hiyo ya Rais, kwa kuwa watendaji wengi
hawafanyi kazi siku za wikiendi licha ya huduma zake
kufanyika siku zote.
Tangu jana asubuhi kumekuwa na video inayosambaa
ikimuonyesha Rais Magufuli akiwa Kivukoni
akitembea kwa miguu ndani ya eneo hilo huku
akishangiliwa na wasafiri waliokuwa wakingoja
kivuko.
Hata hivyo, jitihada za kutafuta mamlaka husika
kueleza kwa undani malengo ya ziara hiyo ziligonga
mwamba baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni
Sefue kutopokea simu.
Ofisa habari wa Wakala wa Ufundi na Umeme
(Temesa) Theresia Mwami, alitaka utafutwe uongozi
wa juu kueleza yaliyojiri kwenye ziara hiyo kwa kuwa
yeye yupo likizo.



Thursday, 18 February 2016

Kambi ya Upinzani bungeni Yaendelea Kumgomea Spika Ndugai

Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu
amesema kambi hiyo haitaongoza kamati za Bunge za Hesabu
za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) hadi
ofisi ya Spika itakapobadilisha uteuzi wa wajumbe wa kamati
hizo.
Kwa mujibu wa mabunge ya Jumuiya za Madola, kamati hizo
huongozwa na wapinzani, lakini tangu Spika wa Bunge, Job
Ndugai afanye uteuzi wa wajumbe, kambi hiyo imesusia
kushiriki uchaguzi kwa kile wanachokiita “kupangiwa
wajumbe”.
Jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema
mazungumzo kati ya ofisi ya spika na kambi hiyo bado
yanaendelea na kusisitiza kwamba uteuzi huo unaweza
kutenguliwa au kuachwa kama ulivyo.
Katika maelezo yake, Lissu alisema licha ya kambi hiyo kuwa
katika mazungumzo na ofisi ya spika, suluhisho
halijapatikana na kusisitiza kuwa msimamo wao upo
palepale.
“Hatujafika popote. Msimamo wetu uko palepale na
hatutakubali kuchaguliwa viongozi wa hizo kamati na CCM,
kama wanafikiria ni lazima iwe wanavyotaka sisi
hatutakubali,” alisema.
Joel aliwahi kunukuliwa na na vyombo vya habari akisema
kuwa kama kambi hiyo itasusia uchaguzi, shughuli za kamati
zitafanywa na makamu wenyeviti ambao wanatokea CCM.
“Ni bora tusiziongoze kabisa kamati hizi. Ukifuatilia utabaini
kuwa katika PAC na Laac tuna wajumbe sita kila kamati kati
ya wajumbe 23, wakati huohuo kamati ya Ukimwi tumepewa
wajumbe 12 kati ya wote 23,” alisema Lissu.
Alisema wajumbe sita waliopo katika kamati ya Laac na PAC
wameteuliwa na CCM na kama kamati hizo zinaongozwa na
upinzani ni lazima wapinzani wajichagulie wajumbe wao,
wakiwamo watakaochaguliwa kuwa wenyeviti. Alisema wabunge
wana haki sawa, lakini hawana uwezo sawa.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), alisema uamuzi wa spika kuwapangia wajumbe
katika kamati hizo hauna nia nzuri na kwamba, huenda ni
mkakati wa ofisi hiyo kuifanya Serikali iwe inapitisha mambo
yasiyofaa bungeni.
Februari Mosi mwaka huu, Kambi ya Upinzani bungeni ilisusia
uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo kwa maelezo kuwa Spika
Ndugai alifanya uteuzi ‘kiholela’ na kuahidi kutoshiriki
mpaka pale watakapopewa idhini ya kupendekeza wenyeviti.



Huyu Hapa Ndio Mwanafunzi Mchina Aliyeshika Nafasi ya Pili Matokea ya Kidato cha Nne Yaliyotoka Jana

Mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne Feza Girls 2015 ,
Mtanzania mwenye asili ya China, Congcong Wang,ameshika
Nafasi ya pili Kitaifa ,amepata Divisheni 1.7 yenye 'B' ya
Kiswahili!


Monday, 8 February 2016

Kimenuka..Mhifadhi wa hifadhi ya Ngorongoro Akamatwa Katika Majangili Tisa Walio Waliotungua Helkopta na Kuua Mzungu Pori la Akiba Maswa

Siku chache baada ya kutokea tukio la majangili katika pori la
akiba Maswa wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, kuitungua
ndege (helikopta) iliyokuwa doria na kuaawa kwa rubani wake
Rodgers Gower (37), watu 9 wamekamatwa kuhusika na tukio
hilo.
Katika watuhumiwa hao mmoja niMhifadhi wa hifadhi ya taifa
ya Ngorongoro kitengo cha Interejensia, ambaye alitajwa kuwa
mhusika Mkuu wa kufanikisha tukio hilo sambamba na
kukamatwa mganga wa jadi.
Akitoa taarifa mbele za waandishi wa habari ofisini kwake
jana, Kamanda wa polisi Mkoani Simiyu Lazaro Mambosasa
alisema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana
na jeshi hilo kufanya kazu usiku na mchana kwa kushirikiana
na wananchi, pamoja na uongozi wa TANAPA.
Kamanda Mambosasa alisema watuhumiwa wote
walikamatwa na kukiri kuhusika na tukio hilo, huku akieleza
kuwa msako mkubwa uliofanywa na jeshi hilo mara baada ya
tukio kutokea chini ya Mkuu wa upelelezi Mkoa Jonathan
Shana.
Alisema katika msako huo baadhi ya watuhumiwa walibainika
kuwa kiungo kikubwa kufanikisha tukio hilo kwa kutoa mbinu
za uharifu, huku wakijihusisha na matukio ya ujangili kwa
muda mrefu.
Aliongeza kuwa baadhi yao walibainika kuwa waganga wa
jadi, ambapo walikuwa wakitoa dawa kwa majangili za kuosha
silaha, ikiwa ni pamoja na kuosha na kusafisha miili yao ili
wasiweze  kukamatwa.
Mambosasa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shija Mjika
(38), Njile Gonga (28) Mhazabe, Masasi Mandago (48) pamoja
na Dotto Pangali (41) , ambao ndio walihusika kutungua
helkopta hiyo.
Wengine ni Iddi Mashaka (49) ambaye Kamanda Mambosasa
alimtaja kuwaMhifadhi wa hifadhi ya taifa ya Ngorongoro
Kitengo cha Intelijensia na ndiye alikuwa kiungo Mkuu wa
tukio hilo.
Aliwataja wengine kuwa ni Mapolu Njige (50) ambaye ni
mganga wa jadi aiyekuwa anatumika kutoa dawa za
kutokamatwa kwa majangili hao, Mwigulu Kanga (40) , Dotto
Huya (45) , Pamoja na Mange Balumu.
Aidha Mambosasa alisema kuwa Mtuhumiwa Dotto Pangali
alikamatiwa katika wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga
mnamo tarehe 7/02/216 na kufanyiwa upekuzi nyumbani
kwake ambapo alikutwa na bunduki aina ya Riffle yenye
namba .7209460 CAR Na.63229.
Mkuu huyo wa polisi alisema Mtuhumiwa huyo alikiri bunduki
hiyo kutumika katika tukio la kuuawa kwa rubani huyo,
ambapo ilibainika kuwa bunduki hiyo inamilikiwa na Mange
Magima ambaye pia amekamatwa.
Alisema msako uliendelea nyumbani kwa Pangali na
kufanikiwa kukamatwa kwa bunduki nyingine aina ya Riffle
Na3478 CAR 458 ikiwa na risasi 6 ambayo ilibainika
kumilikiwa na Nghomango Jilala ambaye mpaka sasa
hajakamatwa.
Alieleza kuwa jeshi hilo liliendelea kupata taarifa ambapo
mnamo tarehe 29/01/2016 walikamatwa Shija Mjika, Njile
Gonga, pamoja na Masasi Mandago wakiwa na meno ya
tembo 2 yakiwa na uzito wa Kilo 31 yakiwa yamefichwa chini
ya daraja katika kijiji cha Itaba.
Aidha Mambosasa alieleza kuwa baada ya kukamatwa kwa
wahusika wote ilibainika kuwa bunduki zilizotumika katika
tukio hilo zinamilikiwa kihalali na watu ambao waliomba
kuzimiliki kwa ajili kujilinda.
“Mbali na tukio hilo bunduki nyingi wamiliki wake
wanawaazimisha majangili kwa ajili ya kutumika kwa uhalifu
pamoja na kuua wanyama ndani ya hifadhi…lakini na hao
wamiliki wanalipwa pesa baada ya uhalifu kufanyika” ,alisema.
Alisema baada ya kubaini hilo kulifanyika msako mwingine
kwa wanaomiliki silaha, ambapo alisema asilimia kubwa
wanaishi karibu na hifadhi, na jumla ya bunduki 27
zimekamatwa na mara baada ya uchunguzi wamiliki
watarudishiwa.
“Tunajiandaa kupeleka zuio la silaha mahakamani ili kubaini
kama wana sifa za umiliki…lakini mbali na hilo sasa
kutaanzishwa oparesheni kwa watu wote wanaomiliki silaha
hasa maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuwanyanganya”, alisema.
Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa upelelezi juu ya tukio hilo
umekamilika na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani
leo Jumanne ili kujibu tuhuma zinazowakabili, ambapo
alioomba mahakama kuharakisha hukumu kwa vile uchunguzi
umekamilika.
Kwa upande wake Mhifadhi mkuu wa Serengeti William
Mwakilema amelipongeza jeshi la polisi ambapo amesema
tukio hilo lilipotokea liliwasikitisha sana kwani hasara
ilipatikana kutokana na kutunguliwa kwa helkopta.
Mnamo tarehe 29/01/2016 saa 11:30 jioni katika eneo la
Gululu lililopo ndani ya hifadhi ya Maswa kata ya Mwangudo
wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, majangili waliipiga risasi
ndege (helkopta) 88HFCG iliyokuwa doria na kusababisha kifo
cha rubani wake Rodgers Gower (37) raia wa uingereza huku
Mwenzake Nicholas Beste (43) raia wa Afrika Kusini
akinususrika kifo


Thursday, 21 January 2016

AWAUA WATOTO WAKE KWA KUWANYWESHA SUMU.

Mama mmoja aitwaye Elizabeti Mugendi, miaka 24, mkazi wa Kamugesi mkoani Mara, anashikiliwa na polisi kwa kosa la kuwanywesha  sumu inayodhaniwa kuwa ni ya kuulia wadudu watoto wake wawili  Francis Steven na  Wanzagi Kitoki.
Baada ya kuwanywesha sumu watoto hao, pia naye alikunywa sumu hiyo na ndipo walikimbizwa katika Hospitali ya Butiama kwa matibabu, wakati wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Butiama watoto hao wawili walifariki dunia, huku mama huyo akinusurika kwa kuendelea na matibabu na hali yake kuendelea kuimarika.
Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi baina ya mtuhumiwa Elizabeti Mugendi na mdogo wake aitwaye Warioba Mugendi, ambaye humpiga mara kwa mara.
Taarifa zinasema hata siku ya tukio, Eliza alipigwa sana na mdogo wake kwa kosa la kuvunja glasi ya maji, ndipo akaamua kunywa na kuwanywesha sumu watoto wake ili waepukane na mateso hayo.
Jeshi la Polisi mkoani humo, linamshikilia Bi Elizabet kwa mahojiano zaidi.

Usinyanyaswe na Polisi..Fanya Haya Uwapo Mikononi Mwa Polisi....Imeandaliwa na Mawakili

Usinyanyaswe na Polisi..Fanya Haya Uwapo Mikononi Mwa Polisi....Imeandaliwa na Mawakili


1. Askari akikuweka chini ya ulinzi muulize kitambulisho ni haki yako.

2. Askari akikukamata akuoneshe kitambulisho chenye muhuri wa mahakama kama anasema ametumwa na mahakama kukukamata, ni haki yako.

3. Askari akikukamata akwambie kwanini anakukamata na anakupeleka kituo gani, ni haki yako.

4. Unaruhusiwa na sheria kukataa kukamatwa hata kutumia nguvu kama hukuambiwa sababu ya kukamatwa.

5. Askari anapokiuka taratibu za ukamataji anageuka na kuwa mhalifu ni haki yako kujikinga naye.

6. Askari haruhusiwi kukuvuta shati, kukukaba koo, kukushika suruali kama hujakataa kutii amri halali.

7. Askari haruhusiwi kuondoka na mtu mwingine baada ya kumkosa mtuhumiwa halisi.

8. Askari haruhusiwi kupekua nyumba ya mtu bila kibali cha kupekua.

9. Askari lazima akuoneshe kibali cha kupekua na ukisome.

10. Kibali kieleze jina la aliyekitoa, kituo kilipotolewa,jina la mtu au sehemu ya upekuzi, au uchanganuzi wa mtu au sehemu.

11. Hairuhusiwi kupekuliwa usiku kuanzia saa 1 jioni mpaka saa 12 asubuhi.

12. Ni haki yako kumpekua askari kabla hajakupekua ili asipandikize kitu.

13. Usipekuliwe nyumbani bila kuwapo kiongozi wa mtaa.

14. Kila kitakachochukuliwa katika upekuzi lazima kiandikwe na askari aweke sahihi.

15. Mali iliyochukuliwa katika upekuzi lazima ibaki salama.

16. Mwanaume haruhisiwi kumpekua mwanamke na mwamke haruhisiwi kwa mwanaume.

17. Unaruhusiwa kukataa kupekuliwa iwapo taratibu hizi hazikufuatwa.

18. Askari haruhusiwi kukutukana wala kukupiga.

19. Unaruhusiwa kutozungumza lolote mpaka unayemuamini afike uwapo chini ya ulinzi, ni haki yako.

20. Usilazimishwe kuongea au kuandika ambacho hutaki, ni haki yako.

21. Usitoe maelezo bila uhakika yatatumika mahakamani yatakuletea shida.

22. Unaruhusiwa kukaa kimya na usizungumze kitu uwapo chini ya ulinzi.

HIZI ZOTE NI HAKI ZAKO, ZILAZIMISHE, USIBEMBELEZE WALA USIZIOMBEMA

Huyu Ndio Jamaa Aliyebuni Jina la Nchi ya Tanzania..Hivi Ndivyo Ilivyokuwa....


Akiwa na umri wa miaka kumi na nane, mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari Mzumbe alishika mkononi gazeti la THE STANDARD[DAILY NEWS, kwa sasa katika maktaba na aliona tangazo lilikuwa linatafuta mtu atakayebuni jina la nchi inayoundwa na nchi mbili za TANGANYIKA na ZANZIBAR, kijana huyu mzaliwa wa Tanga aliamua kulifanyia kazi tangazo hilo ambapo alichukua herufi TAN kutoka neno TANGANYIKA, na herufi ZAN kutoka neno ZANZIBAR, hakuishia hapo, kutokana na uzoefu wake kuwa nchi nyingi za kiafrika ziliishia na herufi za IA, kama vile ETHIOPIA,GAMBIA,TUNISIA,NIGERIA,ALGERIA,SOMALIA,ZAMBIA na NAMBIA,aliona ni vyema basi azitumie herufi za IA ilikupa jina zuri ndipo neno TANZANIA lilipopatikana na kijana yule alituma jina hilo kwenda mamlaka husika.Mohammed Iqbal Dar aliibuka mshindi na alizawadiwa NGAO MAALUMU NA TSH 200. Kwa sasa Bwana Mohammed Iqbal Dar anaishi nchini Uingereza akifanya kazi ya uhandisi wa masuala ya redio. Mohammed Iqbal alizaliwa mwaka 1944 jijini Tanga

Tuesday, 19 January 2016

Breaking News: Jeshi la Polis Lafanikiwa Kukamata Wafanyabiashara Wakongwe wa Madawa ya Kulevya

Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuwanasa wafanyabiashara wakongwe wa dawa za kulevya nchini ambao pia wanadaiwa kufanya biashara haramu za binadamu ambao wamekuwa wakiwasafirisha kutoka nchini kwenda katika nchi zinazozalisha dawa za kulevya.
Magwiji hao wa dawa za kulevya nchini waliotiwa nguvuni na jeshi la polisi ni pamoja na Mohamed Abdallah Omary, Nassoro Suleiman na  meneja wa duka la Tungwe Bureau de Change ambalo hutumika kusafirisha fedha za dawa za kulevya kwenda nchini Pakstani kinyume na sheria.
Taarifa hiyo kamanda Sirro, amesema kwasasa jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha linadhibiti mianya yote ya dawa za kulevya ambapo pia katika msako mkali uliofanyika mwishoni mwa wiki gari zenye namba za usajili T271 DCT, T916 DCL, T593 CEL na T999 DDB  zimekamatwa.
Kamanda Sirro amesema kuwa kumeibuka wimbi la wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha watanzania kuwapeleka nchini Pakstani na kuwaacha kama bondi ili wapatiwe mzigo mkubwa wa dawa za kulevya ambapo wengi wao wamekuwa wakiuawa ambapo amesema jeshi limejipanga kusambaratisha mtandao huo.

Monday, 18 January 2016

Magazeti ya Leo » Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne Ya Januari 19, Ikiwemo ya Lowassa Kutamba Kuwa Mtaiona Dar ya Ukawa


Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne Ya Januari 19, Ikiwemo ya Lowassa Kutamba Kuwa Mtaiona Dar ya Ukawa

Saturday, 16 January 2016

Necta » Tazama Hapa Matokeo ya Kidato cha Pili 2015/16


Baraza la mitiani NECTA limetangaza Matokeo ya kidato cha 2 kwa wanafunzi waliofanya mtihani mwaka jana ambapo wanafunzi 324,068 sawa na 89% kati ya wanafunzi 363,666 waliofanya mtihani wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu.

Wednesday, 13 January 2016

Al Jazeera yafunga runinga Marekani

Shirika la habari la Al Jazeera limefunga matangazo ya Televisheni nchini Marekani ikiwa ni chini ya miaka mitatu tangu kuzindua huduma zake nchini humo.
Al Jazeera imesema kuwa imelazimika kufunga matangazo yake kutokana na ugumu wa mazingira ya soko la televisheni nchini humo. Shirika hilo lenye makao makuu yake Qatar limesema kuwa badala yake linaimarisha na kupanua huduma ya kimtandao katika maeneo ambayo yanaendesha mfumo huo kwa sasa. Taarifa zinasema kuwa Al Jazeera imeshindwa kuwavutia watazamaji wa kutosha nchini Marekani ili kuweza kujitengenezea faida.

BREAKING NEWS:Jeshi la Polisi Latoa Kauli Kali Kwenda kwa Mabenki Kuhusu Ujambazi Dar

Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na Operasheni kali inayoendelea jijini Dar es Salaam Na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.

WAMILIKI wa Taasisi za Kifedha wanatakiwa kujiridhisha kama waajiliwa katika taasisi hizo kama wanahusika kwa njia moja ama nyingine katika uharifu unaohatarisha maisha ya wakazi wa jijini la Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na  Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam leo.

Kamanda Sirro amesema kuwa hatua za makusudi zimechukuliwa katika maeneo mbalimbali hasa ya eneo la Kibiashara la Mlimani City kutokana na matukio mengi ya uporaji  wa fedha kwa kutumia pikipiki.

Pia amesema kuwa pamoja na sheria hizo kuchukuliwa watafanya operasheni maalumu katika eneo hilo na kutafuta namna nzuri ya kuondoa pikipiki katika maeneo hayo.

Katika Operasheni zilizofanywa na Jeshi hilo wamefanikiwa kuwakamata majambazi nane pamoja na kumamata Bunduki mbili aina ya Pump Action ambazo namba zake zilifutwa na kukatwa Mtutu.
Aidha Kamanda Sirro amesema kuwa katika Operasheni hiyo wamemkamata jambazi aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu anayejulikana kama Mkama Hassan mkazi wa Gomgolamboto jijini Dar es Salaam na alipopekuliwa alikutwa na Bastola aina ya Chinese iliyofutwa

Tuesday, 12 January 2016

DPP Adhamiria Kumrudisha Shehe Ponda Issa Ponda Kizimbani... Akata Rufaa Mahakama Kuu Kupinga Kuachiwa Kwake


MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP) ameamua kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya kesi ya uchochezi inayomkabili mwanaharakati wa Kiislamu Shehe Ponda Issa Ponda.
Mwanasheria Mwandamizi katika ofisi ya DPP, Bernard Kongola amesema kuwa Serikali inapinga kuachiwa kwa Shehe Ponda ambaye alishitakiwa kwa makosa ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
“Tayari tumeomba tupatiwe nakala ya hukumu pamoja na nyaraka za mwenendo wa shauri hilo ili upande wa mashitaka tuweze kuandaa rufaa yetu Mahakama Kuu,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, tangu waombe kupatiwa nakala ya hukumu hiyo katika mahakama hiyo ya hakimu mkazi, hakimu ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo bado hajawapatia upande wa mashitaka hukumu ambayo imechapwa.
“Hatujui kuna tatizo gani, maana tunapoomba kupatiwa nakala ya hukumu, hakimu amekuwa anatuambia kwamba bado hawajamaliza kuichapa, kwa kweli hii inashangaza,” alisema.
Novemba 30 mwaka uliopita, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Morogoro, Mary Moyo alimwachia huru Shehe Ponda kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha pasi shaka yoyote mashitaka dhidi ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Wakati kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa, upande wa mashitaka uliita mashahidi wanane kwa lengo la kuthibitisha makosa dhidi ya Shehe Ponda ambaye alikuwa anatetewa na Mawakili wa kujitegemea Juma Nassoro na Abubakar Salum.
Shehe Ponda alifikishwa katika mahakama hiyo Agosti 19, 2013 akikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kukaidi amri ya Mahakama ya Kisutu iliyomtaka awe mhubiri amani katika jamii likiwa ni sharti la kifungo cha mwaka mmoja nje baada ya kumtia hatiani katika kesi ya jinai.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa Shehe Ponda alitenda kosa Agosti 10, 2013 katika eneo la Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege iliyoko katika Manispaa ya Morogoro.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo kiongozi huyo wa kidini alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi ya kuhamasisha jamii kinyume na maelekezo ya mahakama.
Katika mkutano huo Shehe Ponda anadaiwa kusema maneno haya, “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za msikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana.”
Kauli hiyo inadaiwa kwenda kinyume cha amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, iliyotolewa mahakamani hapo na Hakimu Victoria Nongwa, Mei 9, 2013 ambayo ilimtaka ndani ya mwaka mmoja kuhubiri amani na asifanye jambo lolote la uvunjifu wa amani na badala yake ahubiri suala la amani, ambayo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria Namba 124 cha Mwaka 2002.
Shitaka la pili lililokuwa likimkabili Shehe Ponda ni uvunjifu wa sheria Kifungu cha 129 cha Makosa ya Jinai kuwa siku hiyo, alitoa maneno ya uchochezi yaliyohatarisha kuathiri imani za watu wengine.
Katika hati ya shitaka hilo, ilinukuu kauli ya Ponda kuwa “Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu. Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipewe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.”
Shitaka la tatu anadaiwa kutenda kosa kinyume cha sheria kifungu cha 390 na 35 kwa kuchochea maneno dhidi ya wananchi wakati wa kongamano lililofanyika Agosti 10, 2013 Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.

Monday, 11 January 2016

Askofu Kanisa La Anglikana Atimuliwa kwa Ufisadi wa Mamilioni ya Pesa

KANISA la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) lililopo jijini Mwanza, limemtimua rasmi Askofu kanisa hilo, Boniface Kwangu, kutokana na ubadhilifu wa zaidi ya Sh. 600 milioni.

Askofu huyo ni wa pili kutimuliwa na uongozi wa kanisa hilo baada ya mwaka 2007 aliyekuwa Askofu wa dayosisi hiyo, John Changae na yeye kufukuzwa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kitendo ambacho kinaonesha taswira mbaya kwenye kanisa hilo.

Pia Askofu Kwangu aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minane, katika uongozi wake alishawahi kutuhumiwa na waumini wake kuwa anajihusisha na dini ya Freemasons huku wengine walikuwa wakimtuhumu kwamba anatumia nguvu za giza.

Askofu Kwangu na wenzake wanne wanatuhumiwa na kanisa hilo kwa ubadhilifu wa zaidi ya Sh. 600 milioni pamoja na kuendesha kanisa hilo bila kufuata kanuni na taratibu za kanisa hilo kitendo ambacho kimesababisha kutimuliwa kwake.

Askofu Kwangu, anatuhumiwa na upotevu wa Sh. 500 milioni ya shule ya kimataifa ya Isamilo, kuuza gari la dayosisi hiyo, kufukuza wafanyakazi wa kanisa hilo na kusababisha wadaiwe Sh. 60 milioni, kujipatia kiasi cha zaidi ya Sh. 15 milioni kutoka kwa Mhasibu wa kanisa, Sam Wisa, bila kibali.

Akisoma tamko la kumfukuza kazi, Mwenyekiti wa Nyumba ya Wadumu kutoka DVN, Andrew Kashilimu, amesema askofu huyo ameisababishia hasara kanisa hilo zaidi ya Sh. 600 milioni, kutokana na kufanya kazi bila kufuata kanuni na taratibu.

Amesema kuwa askofu Kwangu amekiuka viapo vya uaskofu, katiba ya jimbo, katiba ya DVN na amekiuka maadili na kanuni, kuendekeza matabaka ndani ya wahudumu na waumini, kutoa ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za kanisa.

Amesema katika kikao kilichoketi Septemba 1 mwaka jana, kilithibitisha mambo hayo na kukubaliana kwamba Askofu huyo ajiuzulu kwa afya ya kanisa la Mungu lakini alikaidi maagizo hayo mpaka kutoka kwa tamko hilo.

“Askofu (Boniphace Kwangu) ametumia vibaya madaraka yake na alikuwa anatumia vibaya mali na fedha za kanisa, kwa hali hiyo tusingeweza kuwa na kiongozi wa namna hiyo,” amesema Kashilimu.

Mmoja wa waumini ambaye alikumbwa na fagio la Askofu, Kwangu, Edwar Kibiti, amesema kwamba kutimuliwa kwa kiongozi huyo wa kiroho katika kanisa hilo kutasaidia kurudisha matumaini kwa waumini walio wengi.

Kibiti ambaye pia ni Mchungaji amesema kuwa walipokuwa wakijaribu kuhoji sababu za Askofu Kwangu kuuza mali za kanisa ikiwamo gari alilochangiwa na waumini alikuwa akiwafukuza watu waliotaka kufahamu suala hilo.

“Tulipokuwa tunahoji matumizi ya mali za kanisa tulichokuwa tukiambulia ni kwenda polisi na wengine wafukuzwa, huyu (Askofu Boniphace Kwangu) alikuwa anafanya kazi kwa majungu na mpaka anaondoka alishafukuza wachungaji 19,” amesema Kibiti.

Amesema kuwa baada ya askofu huyo kuona wachungaji wazawa wanaanza kumfuatilia alianza kutafuta wachungaji wengine kutoka nchi mbalimbali hususani kutoka Rwanda, ili kuficha maovu yake anayoyafanya.

Mmoja wa Waumini, Joycelyn Juma, amesema kilichomgharimu askofu huyo ni upungufu wa mambo ya kiuongozi ambayo yamechangia kusababisha kuwepo kwa mwanya wa wizi wa mali na fedha za kanisa hilo.

“Kiufupi nimefurahi sana kwa sababu mambo ya ufisadi ama wizi wa fedha haviendani na mambo ya Mungu na nimefurahi kuona suala hili limefikia mwisho na sasa tutakuwa na amani,” amesema Juma.

Sanjali na kufukuzwa kazi ya Uaskofu DVN, pia uongozi wa kanisa hilo limemfungulia kesi Askofu Kwangu na wenzake wanne, Katibu wa Bodi, James Mtaritinya, Mhasibu wa Shule ya Isamilo, Sam Wisa, Samson Maganga na John Magawa.

Kesi iliyofunguli ni Januari 10 mwaka huu, Mw/Rb/265/2016 ambalo ni jalada la uchunguzi kwa watuhumiwa

Friday, 8 January 2016

BomoaBomoa Yaipasua Kichwa Serikali.......Mwanasheria Wa Nemc Aliyehalalisha Jumba La Mchungaji Rwakatare Afukuzwa Kazi

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU ZOEZI LA KUHAMISHA WAKAZI WA MABONDENI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM

Utangulizi
Nchi yetu ina kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo watu wanaishi kinyume cha sheria, huku wakiharibu mazingira na kuhatarisha maisha yao.  Kutokana na uhaba wa makazi, hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya Jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto Msimbazi.

Serikali za awamu zote, zimekuwa zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa maeneo ya mabondeni wanaoishi katika maeneo hayo kinyume cha sheria lakini mafanikio yamekuwa si ya kuridhisha.

Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo moja ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria za nchi, imeanza jitihada za kuwaondoa wakazi hawa. 

Tuliamua kuanza na Bonde la Mto Msimbazi kwasababu ndiko kwenye watu wengi na athari kubwa.Sababu zetu kuu za kufanya zoezi hili ni kusafisha mabonde na mito katika jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka ni:-

Kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo la Bonde la Mto Msimbazi lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979.

Kupanua uwezo wa mito ya Dar es Salaam ili kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi;Kuzuia milipuko ya magonjwa, hasa ya kipindupindu, hasa wakati wa mvua;

Kuzuia eneo hilo kuendelea kutumika kama maficho ya wahalifu na uhalifu;

Kutoa nafasi kwa Serikali kuandaa na kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;

Utaratibu wa Zoezi
Kabla ya nyumba kubomolewa, taasisi hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote. 

Nyumba ambazo zimethibitika kuwepo katika maeneo yasiyostahili ndio zinawekwa alama X kuashiria kwamba wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya hapo, mkazi hupewa muda wa kubomoa na kuhama mwenyewe.

Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa wenyewe. 

Baada ya hapo, alama huwekwa kuonyesha mpaka wa bonde. Katika zoezi hili, imebainika kwamba sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya mabondeni ni wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu nyingine salama.

 Serikali pia imeweka Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Tathmini ya Zoezi
Jana, terehe 7 Januari 2016, Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais; pamoja na Naibu Waziri wa  Maliasili na Utalii), walifanya mkutano wa kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam. 

Mkutano huo ulipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali, inayoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, ambayo, pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya kubaini makazi yaliyojengwa kinyume cha Sheria katika Bonde la Mto Msimbazi imekamilika. 

Ripoti ilieleza kwamba, hadi sasa, wananchi katika nyumba 774  wamehama na nyumba hizo kubomolewa. Ilielezwa pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa  kuhama, uhakiki kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa. 

Kutokana na uhakiki huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119 walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi. 

Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri walipokea maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi hilo.  

Baada ya tafakuri na mjadala, Mawaziri hao walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa Serikali: -

1.Zoezi la kuwaondoa wananchi waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo hatarishi) litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu kwa wananchi;

2.Katika awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.

3.Kwa wakati huu, watakaohitajika kuhama ni wale tu ambao makazi yao yamo NDANI kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na kwenye KINGO za mto;

4.Wale watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga. Na watumishi wa umma waliowamilikisha maeneo hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria;

5.Serikali, ndani ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji umefanyika.

6.Serikali itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka ili taratibu zinazofuatia zifanyike;

7.Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria. Limeanzishwa dawati la malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupokea malalamiko au maswali kuhusu zoezi hili.

8.Nyumba na majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hayatabomolewa isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini. Wanaoishi katika makazi hayo watapewa miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa;

9.Serikali haina dhamira ya kubomoa mahoteli makubwa ya siku nyingi yaliyo karibu na fukwe katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa mahoteli haya watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.

10.Serikali inaweka uratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii.

11.Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini.

 Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza maisha. Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.

12.  Serikali inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya taarifa za wananchi wanaohitaji msaada maalum wa kibinadamu.

Suala la Mchungaji Getrude Rwakatare
Mkutano ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji Rwakatare.  Ilielezwa kwamba Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume kabisa na Sheria tatu muhimu.  

Pia ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani. 

Wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11 Mei 2015, aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza, kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.  

Makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei 2015. Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo. 

Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa zake zimekwishafikishwa TAKUKURU. 

Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais, iliiagiza Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba “makubaliano” kati yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na njia ya udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe 29 Disemba 2015.

Kuhusu Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano pia ulijulishwa kuhusu hoja inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi mabondeni lakini mradi wa DART umeachwa.

 Mkutano ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa miradi/shughuli zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya mabondeni, na kwamba Waziri mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo zinavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira.

 Mradi wa DART ulipata kibali hicho na una mkataba na Baraza la Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya mazingira zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016

habari zilizopo kwenye magaazeti ya leo

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi Ya Januari 9, Ikiwemo Jide na Namless Wazua Gumzo Picha yao ya Mahaba yatua Kwa Gadner