Friday 26 February 2016

Majina Ya Mawaziri MAJIPU Yakabidhiwa Kwa Waziri Mkuu......Ni Wale Waliogoma Kutangaza Mali Zao

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa majina ya baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri ambao hawajajaza fomu za mali wanazozimiliki kama sheria inavyowataka.

Akizungumza jana kwenye semina ya mawaziri na naibu mawaziri, Kamishina wa Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema viongozi hao wanajua umuhimu wake lakini wanapuuza.

“Sheria hii ya Maadili ya Viongozi wa Umma inajulikana, lakini jambo la kushangaza wapo baadhi ya mawaziri na manaibu ambao hawajajaza, kwa ruhusa yako nitakukabidhi majina yao, sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, hivyo anayekiuka anapaswa kuadhibiwa,” alisema Jaji Kaganda bila kutaja majina hayo.

Kifungu cha 9 cha sheria hiyo kinataka katika kipindi cha siku 30 baada ya kupewa wadhifa, kila mwisho wa mwaka na mwisho wa kutumikia wadhifa wake kiongozi husika anatakiwa kupeleka tamko la maandishi la mali zake.

Sheria hiyo inafafanua kuwa mali hizo ni pamoja na rasilimali zake au mume au watoto wenye umri usiozidi miaka 18 ambao hawajaoa au kuolewa.

Alisema fomu hizo lazima zijazwe na viongozi na wananchi wanaruhusiwa kwenda kuzihakiki wakitoa sababu za msingi, lakini sheria hiyo hairuhusu waende kutangaza na wakifanya hivyo hatua zinachukuliwa dhidi yao.

“Hapo ndipo wananchi wengi huwa hawatuelewi kwa kuwa wanapenda kujua mali ambazo viongozi wao wanamiliki,” alisema.

Alisema Sekretarieti kwa kutambua umuhimu wa viongozi hao kuzingatia sheria na maadili, ndiyo sababu imeandaa semina hiyo baada ya kupata ufadhili kutoka Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID), wakiamini kuwa yatasaidia kuwakumbusha.

0 comments:

Post a Comment