Wednesday 24 February 2016

Mambo Yazidi Kufichuka...Ezekiel Maige Nae Atajwa Ufisadi Ngorongoro

Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii katika serikali
ya awamu ya nne, Ezekiel Maige, jana alitajwa
katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bernard
Murunya ambaye ameshitakiwa kwa matumizi
mabaya ya ofisi.
Katika kesi hiyo, Maige anadaiwa kulipiwa nauli ya
safari ya nje na mamlaka hiyo kwa idhini ya
Murunya, ambaye sasa ni Mbunge wa Afrika
Mashariki.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Sezari Semfukwe,
alidai kuwa Murunya na aliyekuwa Mkurugenzi wa
Fedha na Utawala wa Mamlaka hiyo, Shad Kiambile,
waliidhinisha malipo ya dola 66,890. Alidai kuwa
fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya safari ya Maige na
msaidizi wake aliyetajwa kwa jina la E. Muyungi na
Murunya mwenyewe.
Semfukwe, ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa
mamlaka hiyo, alidai kuwa Murunya na Kiambile,
ndio walioidhinisha madokezo kwa ajili ya malipo
hayo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Hamidu Sembano,
akisaidiana na Rehema Mteta, mbele ya Hakimu wa
Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda,
Semfukwe alidai kuwa utaratibu wa maombi ya
safari, unatokana na maelekezo ya mkuu wa idara
na kujaza fomu inayoonyesha anakwenda wapi na
kwa muda gani.
Sambamba na hilo, alidai kuwa aina zingine za safari
zinahusisha watu wa nje ambao, si waajiriwa wa
NCAA kwa dokezo la mkuu wa idara au shirika.
Alidai kuwa alitoa hundi ya malipo namba 309/0238
ya Septemba 9/2011, ambayo ilikuwa na dokezo la
safari kutoka kwa Murunya kwenda kwa Mkuu wa
Kitengo cha Fedha. Pia alitoa hundi ya malipo
nyingine iliyokuwa ikionyesha imelipwa dola
zaMarekani 66,890 kwa kampuni ya Wakala wa
Usafirishaji ya Cosmas.
Aliendelea kudai kuwa hundi za malipo namba
310/0379 ya Oktoba 29, 2011 na ankara namba 5609
ya Septemba 7,  2011 zililipwa kwa Antelope Tours &
Traveling kwa ajili ya tiketi za Murunya, Muyungi na
Maige kwa malipo ya dola za Marekani 66,890 (zaidi
ya Sh. milioni 133).
Shahidi hiyo alidai kuwa kumbukumbu ya kitabu cha
malipo ya hundi inaonyesha hundi namba 002758 na
002755 za Septemba 9, 2011 zililipwa kwa kampuni
ya Cosmas Travelling Agent na zilitiwa saini na
Kiambile na Murunya.
Hata hivyo, wakati shahidi huyo akitoa vielelezo hivyo
mahakamani hapo ili vitumike kama ushahidi,
malumbano ya kisheria yaliibuka baina ya mawakili
wa pande zote.
Malumbano hayo yaliibuka baada ya upande wa
washtakiwa, ukiongozwa na wakili Amani Mirambo,
kutaka kujua ni vielelezo vingapi au vya aina gani
ambavyo upande wa mashtaka unavileta.
Hatua hiyo ilisababisha malumbano ya kisheria hivyo
kumfanya hakimu kuahirisha kesi kwa dakika 10.
Baada ya muda huo, alirejea mahakamani baada ya
dakika hizo na kuwahoji.
Baada ya kuhoji pande zote mbili, kutokana na
malumbano ya kisheria, Hakimu alikatizwa na Wakili
wa Serikali Hamidu Simbano, aliyemwomba
kuahirisha kesi hiyo na kutaja tarehe nyingine ya
washtakiwa kusomewa maelezo yao ya awali.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Rehema Mteta,
aliwasomea maelezo ya awali juu ya tuhuma za
matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha
mamlaka hiyo kupoteza dola 66,890 (Sh.
133,780,000).
Mteta aliwataja washitakiwa, mbali na Murunya na
Kiambile, kuwa ni Meneja Utalii wa mamlaka hiyo,
Veronica Funguo na Salha Issa ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Cosmas Travelling Agent.



0 comments:

Post a Comment