Friday, 21 August 2015

Wasanii Wazindua Kampeni Kuipigia Debe CCM na Tamasha la 'Mama Ongea na Mwanao'


WASANII ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameandaa Tamasha kubwa kuzunguka nchi nzima kwa pamoja na kukinadi chama hicho tawala pamoja na Sera zake ili kiweze kushinda Uchaguzi Mkuu onaotarajia kufanyika Oktoba Mwaka huu (2015).
 
Tamasha hilo litakalojulikana kama “MAMA ONGEA NA MWANAO 2015″ limeandaliwa na baadhi ya wasanii makada wa CCM wapatao 250 ambao watazunguka mikoa zaidi ya 10 kukipigia kampeni chama hicho tawala ili kiweze kupewa ridhaa tena na Wananchi ya kuendelea kuongoza nchi.
 
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Mwenyekiti Msaidizi wa tamasha hilo, Wema Sepetu alisema madhumuni ya tamasha la Mama Ongea na Mwanao 2015 ni kulinda mazuri yote yalioasisiwa na CCM kupitia viongozi wake akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume.
 
Msanii Sepetu akiyataja masuala hayo yalioasisiwa na CCM kupitia viongozi hao kuwa ni pamoja na amani na utulivu uliopo hadi sasa, maendeleo ya kijamii na kiuchumi yalioletwa hadi sasa, masuala ambayo yanastahili kuendelezwa na wala si kubezwa.
 
Tamasha hilo linajumuisha wasanii kama Odama, Davina, Wastara Juma, Keisha, Wellu Sengo (Matilda), Bi. Mwenda, Mama Lolaa, Mama Nyamayao, Herieth Chumila, Thea, Maya, Chuchu Hans, Steve Nyerere pamoja na wasanii wengine wengi.
 
Aidha alisema kupitia tamasha hilo wasanii hao pamoja na wenzao watazunguka katika mikoa zaidi ya 10 kwa pamoja kufanya kampeni kumnadi mgombea wa urais kupitia CCM, Dk. John Pombe Magufuli, mgombea Mwenza, Samia Hassan Suluhu pamoja na viongozi wengine ngazi mbalimbali wanazogombea kupitia chama cha Mapinduzi.
 
Madhumuni ya tamasha la Mama Ongea na Mwanao 2015 ni kulinda mazuri yote yalioasisiwa na CCM kupitia viongozi wake akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume ambayo bila amani mama awezi kujifungua salama, Bila mama hakuna familia, amani inapotoweka mama hawezi kukimbia kilometa kadhaa na kuiacha familia yake, bila mama hakuna ujasiliamali, mama ni kimbilio la baba, kaka, dada na watoto…ikumbukwe kuwa mama ndio mpiga kura ndio maana tunasema mama ongea na mwanao,” alisema Wema Sepetu.
 
“Na leo hii kuanzia sasa tunatambulisha kampeni yetu tunayoifanya kuhamasisha vijana, kinamama, kinababa, mashabiki wetu wale wote wenye sifa za kupiga kura wapige kura kwa kumchagua kiongozi bora anayetoka Chama Cha Mapinduzi…chagua Dk. Magufuli, Samia Suluhu, wabunge na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi,” alisema Sepetu.
 
Aidha wasanii hao wamempongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kuongoza vizuri vikao vyote vya chama hicho hadi kupatikana kwa mgombea bora wa urais kupitia chama hicho (Dk. Magufuli), hivyo kuwataka wanaCCM wote ambao waligombea na hawakupata nafasi kuungana na kukitumikia chama.
 
“…Mimi Wema Abraham Sepetu nikiwa na baadhi ya wasanii wenzangu ambao tuligombea tunasema muda bado tunao na siku tunazo kwa kukitumikia chama tukipewa ridhaa kwa njia yoyote na kwa nafasi yoyote ndio maana hatuja teteleka tupo imara kuwatumikia wananchi katika nafasi nyingine ndani ya CCM,” alisema Sepetu.
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mratibu wa Tamasha la MAMA ONGEA NA MWANAO 2015 litakaloipigia kampeni CCM, Steve Mengele a.k.a Steve Nyerere akizungumza na waandishi wa habari leo juu ya tamasha hilo.
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mratibu wa Tamasha la MAMA ONGEA NA MWANAO 2015 litakaloipigia kampeni CCM, Steve Mengele a.k.a Steve Nyerere akizungumza na waandishi wa habari  juu ya tamasha hilo.
Mwenyekiti Msaidizi wa Tamasha la MAMA ONGEA NA MWANAO 2015 litakaloipigia kampeni CCM, Wema Sepetu (kulia) akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam juu ya tamasha na kampeni zao. Kutoka kulia ni Wellu Sengo (Matilda) na Yobnesh Yusuph (Batuli).
Mwenyekiti Msaidizi wa Tamasha la MAMA ONGEA NA MWANAO 2015 litakaloipigia kampeni CCM, Wema Sepetu (kulia) akizungumza na wanahabari  jijini Dar es Salaam juu ya tamasha na kampeni zao. Kutoka kulia ni Wellu Sengo (Matilda) na Yobnesh Yusuph (Batuli).
Mwenyekiti Msaidizi wa Tamasha la MAMA ONGEA NA MWANAO 2015 litakaloipigia kampeni CCM, Wema Sepetu akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam juu ya tamasha na kampeni zao. Kulia ni Yobnesh Yusuph (Batuli) na kushoto ni Steve Mengele a.k.a Steve Nyerere wakiwa katika mkutano huo.
Mwenyekiti Msaidizi wa Tamasha la MAMA ONGEA NA MWANAO 2015 litakaloipigia kampeni CCM, Wema Sepetu akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam juu ya tamasha na kampeni zao. Kulia ni Yobnesh Yusuph (Batuli) na kushoto ni Steve Mengele a.k.a Steve Nyerere wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya wasanii na makada wa CCM ambao watajumuika katika tamasha la MAMA ONGEA NA MWANAO 2015 litakaloipigia kampeni CCM wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano na waandishi wa habari.



0 comments:

Post a Comment