MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP) ameamua kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya kesi ya uchochezi inayomkabili mwanaharakati wa Kiislamu Shehe Ponda Issa Ponda.
Mwanasheria Mwandamizi katika ofisi ya DPP, Bernard Kongola amesema kuwa Serikali inapinga kuachiwa kwa Shehe Ponda ambaye alishitakiwa kwa makosa ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
“Tayari tumeomba tupatiwe nakala ya hukumu pamoja na nyaraka za mwenendo wa shauri hilo ili upande wa mashitaka tuweze kuandaa rufaa yetu Mahakama Kuu,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, tangu waombe kupatiwa nakala ya hukumu hiyo katika mahakama hiyo ya hakimu mkazi, hakimu ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo bado hajawapatia upande wa mashitaka hukumu ambayo imechapwa.
“Hatujui kuna tatizo gani, maana tunapoomba kupatiwa nakala ya hukumu, hakimu amekuwa anatuambia kwamba bado hawajamaliza kuichapa, kwa kweli hii inashangaza,” alisema.
Novemba 30 mwaka uliopita, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Morogoro, Mary Moyo alimwachia huru Shehe Ponda kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha pasi shaka yoyote mashitaka dhidi ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Wakati kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa, upande wa mashitaka uliita mashahidi wanane kwa lengo la kuthibitisha makosa dhidi ya Shehe Ponda ambaye alikuwa anatetewa na Mawakili wa kujitegemea Juma Nassoro na Abubakar Salum.
Shehe Ponda alifikishwa katika mahakama hiyo Agosti 19, 2013 akikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kukaidi amri ya Mahakama ya Kisutu iliyomtaka awe mhubiri amani katika jamii likiwa ni sharti la kifungo cha mwaka mmoja nje baada ya kumtia hatiani katika kesi ya jinai.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa Shehe Ponda alitenda kosa Agosti 10, 2013 katika eneo la Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege iliyoko katika Manispaa ya Morogoro.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo kiongozi huyo wa kidini alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi ya kuhamasisha jamii kinyume na maelekezo ya mahakama.
Katika mkutano huo Shehe Ponda anadaiwa kusema maneno haya, “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za msikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana.”
Kauli hiyo inadaiwa kwenda kinyume cha amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, iliyotolewa mahakamani hapo na Hakimu Victoria Nongwa, Mei 9, 2013 ambayo ilimtaka ndani ya mwaka mmoja kuhubiri amani na asifanye jambo lolote la uvunjifu wa amani na badala yake ahubiri suala la amani, ambayo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria Namba 124 cha Mwaka 2002.
Shitaka la pili lililokuwa likimkabili Shehe Ponda ni uvunjifu wa sheria Kifungu cha 129 cha Makosa ya Jinai kuwa siku hiyo, alitoa maneno ya uchochezi yaliyohatarisha kuathiri imani za watu wengine.
Katika hati ya shitaka hilo, ilinukuu kauli ya Ponda kuwa “Serikali ilipeleka Jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu. Lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipewe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.”
Shitaka la tatu anadaiwa kutenda kosa kinyume cha sheria kifungu cha 390 na 35 kwa kuchochea maneno dhidi ya wananchi wakati wa kongamano lililofanyika Agosti 10, 2013 Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
0 comments:
Post a Comment