KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, leo anatarajia kufichua siri ya mazungumzo ya kusaka suluhu, baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kufutwa mwaka jana.
Maalim Seif, anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari leo saa tano asubuhi kueleza hatima ya mazungumzo ya kisiasa ya kutafuta mwafaka Zanzibar
“Maalim Seif kesho (leo), atazungumza na wahariri na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano Zanzibar,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana.
Seif anachukua uamuzi huo wakati hali ya kisiasa visiwani humo ikizidi kuwa ngumu kwa pande zote, licha ya Rais Dk. John Magufuli kuahidi kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Maalim Seif anajitokeza leo, wakati wiki iliyopita Rais Magufuli alikutana na viongozi wastaafu, ambao kwa pamoja walizungumza mambo mazito ya kitaifa pamoja na kutakiana heri ya mwaka mpya.
Wiki iliyopita Rais Dk. Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alimhakikishia kumpa ushirikiano atakapohitajika kufanya hivyo.
Katika kumhakikishia kuwa yuko tayari kufanyakazi atakayomtuma, taarifa za ndani zinaeleza kuwa moja ya jambo kubwa ambalo Mkapa anaweza kulisimamia ni suala la kusaka suluhu ya Zanzibar.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Mkapa alisema lengo la mkutano huo ni kumpongeza Rais Dk. Magufuli kwa dhamana aliyopewa na Watanzania na kumtakia heri ya mwaka mpya.
Mkapa alimhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wowote na kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.
Licha ya Mkapa, Rais Magufuli pia alikutana na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ambaye alikabidhi baadhi ya nyaraka kwa Rais Magufuli.
Kikwete alikabidhiwa nyaraka hizo zinazohusiana na mgogoro huo na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 4, mwaka jana.
Inaelezwa kuwa Maalim Seif alikabidhi nyaraka mbalimbali, zikiwamo fomu za matokeo ya Uchaguzi Mkuu kwa vituo vyote vya Zanzibar
Monday, 11 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment