Monday 22 February 2016

Magufuli Alivyotinga Kivukoni na Magari Yenye Namba za Kawaida Bila Taarifa..

Rais John Magufuli ameendelea kufanya ziara za
kushtukiza, baada ya kutembelea ofisi za Kivukoni
Dar es Salaam kimyakimya juzi jioni kuangalia
mwenendo wa utoaji huduma za vivuko.
Mashuhuda waliokuwepo eneo hilo Jumapili jioni
wakati Rais anafanya ziara hiyo, walieleza mtindo
alioingia nao Dk Magufuli ulikuwa ni wa kawaida na
vigumu kwa mwananchi wa kawaida kung’amu uwapo
wa Rais.
Mfanyabiashara wa eneo hilo, Sharif Mkamba
alisema Rais Magufuli aliingia saa 11 jioni akiwa na
msafara wa magari matatu ya kawaida yaliyokuwa
na namba za kiraia.
“Hakukuwa na king’ora chochote kama tulivyozoea
bali ulikuwa ni msafara wa kimya kimya. Aliingia
moja kwa moja kwenye zile ofisi na alitumia kati ya
dakika 10 hadi 15 kabla ya kutoka,” alisema
Mkamba.
Said Likoko alisema kuwa baada ya kugundua kati ya
magari matatu alikuwepo Rais, walisogea kufuatilia
kwa kina kwa kuwa haijazoeleka na walitegemea
huenda baadhi ya watumishi wangewajibishwa.
“Aliteremka na kumuuliza aliyemkusudia na taarifa
tulizozipata jana zinadai hakumkuta huyo bosi, sijui
ni meneja au ofisa sisi hatujui,” alisema Likoko
ambaye hujishughulisha pia na biashara ndogondogo
eneo la kivukoni.
Likoko alisema pamoja na kwamba aliingia kimya
kimya, Rais Magufuli hakusita kuwasalimia wasafiri
waliokuwa wakisubiri kivuko wakati alipofanya ziara
hiyo.
Alieleza kuwa kama wananchi walifurahishwa na
hatua hiyo ya Rais, kwa kuwa watendaji wengi
hawafanyi kazi siku za wikiendi licha ya huduma zake
kufanyika siku zote.
Tangu jana asubuhi kumekuwa na video inayosambaa
ikimuonyesha Rais Magufuli akiwa Kivukoni
akitembea kwa miguu ndani ya eneo hilo huku
akishangiliwa na wasafiri waliokuwa wakingoja
kivuko.
Hata hivyo, jitihada za kutafuta mamlaka husika
kueleza kwa undani malengo ya ziara hiyo ziligonga
mwamba baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni
Sefue kutopokea simu.
Ofisa habari wa Wakala wa Ufundi na Umeme
(Temesa) Theresia Mwami, alitaka utafutwe uongozi
wa juu kueleza yaliyojiri kwenye ziara hiyo kwa kuwa
yeye yupo likizo.



0 comments:

Post a Comment