Monday 22 February 2016

Profesa Ibrahim Lipumba Aibuka....Amtaka Rais Magufuli Atangaze Mshahara Na Marupurupu Yake

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba amemtaka Rais John Magufuli atangaze
mshahara na marupurupu yake, kwa kuwa
amejivisha joho la kuwa Rais wa wanyonge.
Profesa Lipumba amelieleza gazeti la Mwananchi
kuwa Rais Magufuli amejipambanua kuwa kiongozi
anayeguswa na matatizo ya wanyonge, hapendi
makuu, anahimiza ukusanyaji wa mapato ya Serikali
na matumizi mazuri ya fedha za umma, lakini
watanzania hawajui mshahara wake ni kiasi gani
Profesa huyo aliyejikita katika masuala ya uchumi,
alirejea mijadala mbalimbali iliyowahi kuibuliwa
kuhusu mshahara wa Rais, ikiwamo ule uliyowahi
kuibuliwa mwaka 2013 na Zitto Kabwe, wakati huo
akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kuwa Rais
analipwa Sh32 milioni kwa mwezi.
Pia alirejea taarifa iliyochapishwa na Mwananchi,
Julai 27, 2015, iliyoandikwa kutoka katika mtandao
wa African Review kuwa Rais mstaafu Jakaya
Kikwete ni wa nne miongoni mwa marais wa Afrika
kwa kupata mshahara mkubwa wa dola za Marekani
192,000 kwa mwaka sawa na dola 16,000 kwa mwezi,
ambayo ni sawa na Sh32 milioni kwa mwezi. Hadi
jana jioni, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na
Sh2,187.
“Taarifa ya Ikulu ilikanusha vikali habari
zilizochapishwa na Mwananchi. Ikulu ilieleza kuwa
habari hizo siyo za kweli. Hata hivyo, haikueleza
mshahara wa Rais na marupurupu yake ni kiasi
gani?
Pia, katika mjadala wa mshahara wa Rais, Naibu
Spika wa Bunge lililopita ambaye ndiye Spika wa sasa,
Job Ndugai alinukuliwa akieleza kuwa mshahara wa
mtu ni siri yake.
Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
utumishi wa Umma wa wakati huo, Celina Kombani
(kwa sasa ni marehemu) alisema kuwa ni kosa
kutangaza mshahara wa Rais.
“…Kwa hivi sasa Rais Magufuli atangaze mshahara
na marupurupu yake na kama mapato yake ni Sh32
milioni kwa mwezi, basi ajitolee alau nusu ya mapato
hayo kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Hatua
hii itaimarisha taswira inayojengeka barani Afrika
kuwa yeye ni Rais wa wanyonge,” amesema Lipumba.
Wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam wiki
iliyopita, Rais Magufuli aliwataka mawaziri, naibu
mawaziri na makatibu wakuu wachangie Sh1 milioni
katika mishahara yao kuchangia elimu.
Pia Rais alieleza kuwa yeye mwenyewe, makamu wake
na waziri mkuu watachangia Sh6 milioni kila mmoja,
ili zifike Sh100 milioni kusaidia changamoto za elimu
bure Mkoa wa Dar es Salaam.
Kutokana na tangazo hilo, Profesa Lipumba alisema,
“Ikiwa Sh6 milioni zitakatwa katika mshahara wake
wa mwezi mmoja ni wazi mshahara wake na ule wa
makamu wake na waziri mkuu ni zaidi ya Sh6 milioni
kwa mwezi.
“Mishahara na marupurupu ya viongozi wa Tanzania
hayako wazi. Watanzania hawajui kila mwezi Rais,
Makamu wa Rais na viongozi wakuu wa Serikali
wanalipwa kiasi gani? Malipo ya wabunge pia hayako
wazi?” alihoji.
Profesa Lipumba ambaye amewahi kuwa msaidizi wa
Rais katika masuala ya uchumi kati ya mwaka 1991
na 1993, alisema kwa kuwa Rais Magufuli amejivisha
joho la kuwa Rais wa wanyonge, anawajibika
kuwaeleza Watanzania mshahara na marupurupu
yake.
“Ikiwa mshahara ni mkubwa sana achukue hatua za
kuupunguza kama alivyofanya Mwalimu Nyerere
mwaka 1965.”
Hata hivyo, alisema kifungu cha Katiba cha 43 (2)
kinaeleza kuwa mshahara na malipo mengineyo yote
ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa
bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa
masharti ya Katiba.
Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli akitaka
kupunguza mshahara wake itabidi kwanza abadilishe
kifungu hicho cha Katiba.
“Anaweza kujitolea mchango wa kudumu
utakaokatwa kutoka kwenye mshahara wake
kusaidia sekta ya afya au elimu,”alisema.
Profesa Lipumba ambaye ni mshauri wa Benki ya
Dunia (WB) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika
masuala ya uchumi, alisema ili kuimarisha utawala
bora ni muhimu uongozi ulio madarakani utumie
mamlaka waliopewa kwa manufaa ya Taifa.
“Mishahara na marupurupu ya viongozi yawe wazi na
yaamuliwe na kupangwa na taasisi iliyo huru. Kuweka
utaratibu ulio wazi wa kuamua mishahara na
marupurupu ya viongozi wa umma wakiwamo Rais na
makamu wake, mawaziri, wabunge, majaji, makatibu
wakuu na viongozi wengine,”alisema.
Alisema ni muhimu katika ujenzi wa utawala bora,
uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa umma kwa
wananchi wanao waongoza.
“ Inasemekana mshahara wa mbunge katika Bunge
lililopita ulikuwa Sh3.4 milioni kila mwezi.Pia mbunge
alilipwa Sh8.2 milioni, nyingine kama posho ya jimbo,
gharama za ofisi, mafuta, malipo ya wasaidizi wake
na dereva.
“Vile Vile, mbunge anapohudhuria kikao cha Bunge
alilipwa posho ya Sh80,000 za kujikimu, Sh50,000 za
mafuta ya gari na Sh200,00 za kuhudhuria kikao cha
Bunge, jumla ni Sh330,000 kwa siku.
“Posho ya siku moja ya mbunge ni zaidi ya mara mbili
ya kima cha chini cha mshahara wa Serikali kwa
mwezi mzima ambacho ni Sh150,000. Mishahara
inakatwa kodi, marupurupu hayakatwi kodi,”alisema.


0 comments:

Post a Comment