Thursday, 30 July 2015

PROF.MWANDOSYA KUHAMIA CHADEMA, asema Lowassa ni maarufu atakayempuuza apuuzwe yeye



Mwandosya asema Lowassa ni maarufu atakayempuuza apuuzwe yeye
SIKU moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza rasmi kuondoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameibua mjadala mzito kila kona ya nchi.
Lowassa alijiunga na chama hicho kinachounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jijini Dar es Salaam juzi huku akisema CCM siyo baba wala mama yake, hivyo alitangaza kukihama.
Vyama vingine vinavyounda umoja huo ni National League Democracy (NLD) kinachoongozwa na, Dk. Emmanuel Makaidi, Chama cha Wananchi (CUF) kinachoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba na NCCR-Mageuzi chini ya uongozi wa James Mbatia.
Baadhi ya watu wamepongeza uamuzi wa Lowassa kujiondoa CCM kwenda Chadema kwamba ni wa kijasiri na utafungua milango kwa vigogo wa chama hicho waliokuwa na hofu kuhama, huku wengine wakiuponda wakisema hautaweza kukiyumbisha chama hicho tawala.
Kilimanjaro wanena
Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Bazili Lema alisema kitendo cha Lowassa kuhamia chama chao amekipokea kwa mikono miwili, kutokana na kuwa na imani naye na kusema ujio wake utaleta juhudi za kuhakikisha wanaiondoa CCM madarakani.
Lema alisema ukiachilia juhudi za kuongeza nguvu katika kuiondoa CCM, lakini pia kwa viongozi waliokaa katika vyama vya upinzani wanajua ilivyo kazi ngumu kwa mtu kutoka CCM, na kujiunga na chama kingine cha siasa, kwani inahitaji kujitoa sadaka, kujituma kwani CCM ni chama dola kinachotumia ubabe katika kuendesha siasa.
Alisema CCM ni ngome ya wezi na mafisadi katika nchi hii, na kudai kuwa ufisadi haupo kwa mtu mmoja mmoja badala yake upo ndani ya chama.
“Akitokea mmoja anatoka kwenye bahari ya CCM, na kuingia katika vyama vya upinzani maana yake yuko tayari kusaliti ufisadi wa CCM, hivyo ni ushindi kwa wanaopigania haki, wanaopigana kupambana na ufisadi wamembatiza na kumwondolea dhambi ya ufisadi aliyokuwa nayo CCM,” alisema Lema.
Lema alidai kuwa Lowassa kujiunga na Chadema yuko tayari kuhakikisha anapigania kuondoa ufisadi ndani ya nchi yetu, na kudai kuwa panya aliyeamua kuhamia chumba cha paka, na kama hatakuwa na tabia za paka hawezi kuishi.
Alisema kilichomuondoa Lowassa ni tabia za CCM kuoneana, kudhulumiana, kunyanyasana, ununuzi wa kura zimemfika shingoni na kushindwa kuvumilia.
Aliongeza kuwa CCM walikuwa wakiangaika usiku na mchana kuhakikisha kuwa Lowassa hajiungi na Chadema, lakini sasa amejiunga na Chadema, hivyo wanachofanya si kupambana na Lowassa na badala yake wanapambana na Chadema.
Katibu CCM
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Deogratius Rutt alisema miongoni mwa watu walioamini na kupewa heshima kubwa ni Lowassa na hakutegemewa kufanya kitendo kama hicho.
Rutt alisema anawashangaa Ukawa kwa kitendo cha kumpokea Lowassa, kwani walikuwa mstari wa mbele kuwaambia wananchi kuwa Lowassa fisadi, mwizi iweje leo wanampokea na kudai Lowassa jembe.
Alisema Chadema walidai kuwa hawawezi kupokea makapi kutoka CCM, lakini mtu aliyekuwa akigombea nafasi ya urais kupitia CCM na kukosa sifa wao ndiyo wanamchukua.
Kuhusu kupasuka kwa chama baada ya Lowassa kuhamia Chadema, Rutt alisema chama hakikubebwa na Lowassa, hivyo kutoka kwake hakuwezi kusababisha mpasuko na kwamba kila mmoja ana uhuru wake wa kuamua anakwenda chama gani.
Elizabeth Juma alisema kitendo cha Lowassa kuhamia chama kingine ni haki yake, lakini pia wananchi wana wajibu wa kuchagua kiongozi atakayewaletea maendeleo na si kuangalia anapendwa na watu au anatokea chama gani ili mradi anafaa kuwaongoza.
Jamal Rajabu alisema kitendo cha Lowassa kuhama chama amefurahi na kusema itakuwa fundisho kwa CCM kutenda haki katika kura zao za maoni na si kumbeba mtu kwa kuwa wanajua watapata manufaa ndani ya chama hicho, kwani wananchi hawataki kuchaguliwa Rais.
Mbeya wafunguka
Mwenyekiti wa Chama cha Wazabuni Mkoa wa Mbeya, Yahaya Lema ameunga hatua ya Lowassa kujiunga upinzani kwa madai kutaimarisha demokrasia ya kweli hususan kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Alisema uamuzi wa kiongozi huyo wa juu kutoka CCM haupaswi kuchukuliwa kwa mtazamo hasi, bali kama changamoto ya kidemokrasia na kwamba utasaidia kuimarisha na kuleta uwiano wa kisiasa nchini.
Mwenyekiti wa APTT-Maendeleo, Godfrey Mwandulusya kwa upande wake alisema kuondoka kwa kiongozi huyo kumetokana na ufinyu wa demokrasia ndani ya vyama vya siasa nchini, kwani haki yake iliporwa kwa kuwa chombo kilichomuengua hakikuwa na mamlaka hayo kwa mujibu wa kanuni za chama chake cha zamani.
Aliongeza kuwa kutokana na hatua hiyo ya Lowassa kujiunga upinzani kutashuhudia uchaguzi wenye kinyang’anyiro kikali dhidi ya chama tawala na vile vya upinzani vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kamishina wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Mbeya, Eddo Mwamalala alisema,”binafsi napongeza uamuzi mgumu wa Lowassa kujiunga Ukawa kupitia Chadema, amefungua milango mipana ya demokrasia nchini na kuwatoa minyororo wale waliokuwa wanadhani siasa za upinzani ni uadui,” alisema.
Aliongeza kuwa kuhama kwa Lowassa kutaleta tija ya vyama na watawala wajao kwani kitendo chake hicho kinaashiria kizazi kilichopo kiamue hatima ya taifa lijalo.
Ezekiel Kipigapasi, mkazi wa Mbalizi jijini Mbeya, alisema Lowassa kafanya uamuzi sahihi kwa malengo ya kisiasa aliyojiwekea, lakini si rahisi kutimia kwa kuwa atahitaji kuungwa mkono na wafuasi wake aliowaacha ndani ya CCM.
“Labda kama ataondoka na sehemu kubwa ya wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya, lakini ninavyoona si rahisi, hivyo kwa kuwa CCM na mifumo yake ya kiutawala haitakubali kuona wanadhalilika kwa kuruhusu kupoteza katika uchaguzi mkuu,” alisema Kipigapasi.
Kipigapasi alisema hata kama idadi kubwa ya wana-CCM walikuwa wanamuunga mkono kwenye mchakato wa kura za ndani za maoni ya chama hicho hawatakuwa tayari kumfuata kiongozi huyo kwa kuwa wengi wao wana hofu ya kupoteza nafasi zao.
Omar Mruma yeye alisema siasa za sasa ni biashara, kila mtu anaangalia wapi anaweza kufanikiwa kirahisi, hivyo uamuzi wa kiongozi huyo unalenga zaidi maslahi yake binafsi na si taifa au wananchi.
Arusha usipime
William Laizer alisema hatua ya Lowassa kuhama CCM ni haki yake ya kikatiba.
Alifafanua kwamba mpasuko wowote utakaotokea ndani ya CCM utakuwa umesababisha na viongozi wachache wa chama hicho waliosimamia mchako wa kumpata mgombea urais ndani ya chama hicho.
Elizabeth John alisema alichotendewa Lowassa si cha haki ndani ya CCM kwa kutambua kuwa CCM ni chama ambacho siku zote kimekuwa ni chama cha kutumia demokrasia katika utoaji wa uamuzi wake wote.
“Uamuzi uliofanyika Dodoma wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi ya urais ndani ya CCM ulifanywa na kikundi cha watu wachache bila hata kuwahoiji watia nia wote waliojitokeza nguvu ya udikteta ilitumika zaidi wakati wa mchakato huo,” alisisitiza Elizabeth John.
Anton Mathayo alisema Lowassa ana akili timamu, ana uamuzi wa utu uzima alichoamua ni haki yake na wala hakulazimishwa na mtu yeyote.
Eliewaha Mmbaga kutoka Kijiji cha Mhezi alisema Tanzania inahitaji kiongozi ambaye ataisaidia nchi kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo.
Mkazi wa Arumeru, Monica Charles aliema Lowassa angepaswa kuwa mtulivu licha ya kwamba CCM si baba yake wala mama yake, lakini akumbuke hicho ndicho chama kilichomlea maisha yake yote akiwa katibu msaidizi.
Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Masaera, Celina Minja alisema Lowassa asingepaswa kuhama chama bali alipaswa kukubali yote yaliyotokea, kwani hatua ya kwenda upinzani ni kukidhalilisha CCM.
Alisema wapo viongozi wengi waliojitosa nafasi hiyo wa ngazi ya juu katika taifa lakini wamekubaliana na matokeo.
Tabora wamvulia kofia Lowassa
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Tabora, Idd Shaaban Kapama alisema kila mtu ana haki ya kidemokrasia kuamua aende chama gani pasipoingiliwa na mtu yeyote yule hasa anapoona hajatendewa haki na chama chake.
Alieleza wazi kuwa kama atapitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kugombea urais mwaka huu watakipa wakati mgumu CCM katika uchaguzi ujao kwani Lowassa anakubalika na watu wengi na ana ushawishi wa kisiasa.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Tabora, Athuman Balozi alisema uamuzi wa Lowassa kuachana na chama chake ni wa busara, kwani CCM si chama pekee hapa nchini na si baba yake wala mama yake kama alivyodai.
Kada na Mhamasishaji Mkuu wa Chadema Mkoa wa Tabora, Daudi Elisha alipongeza uamuzi huo na kueleza kuwa sasa Ukawa wamepata jembe la nguvu na kutoa mwito kwa makada wengine wanaotendewa ndivyo sivyo ndani ya CCM kujiunga na chama hicho ili kuongeza nguvu zaidi ya kukiondoa madarakani chama tawala.
“Lowassa hana ubaya wowote na wala si fisadi ndiyo maana hakushtakiwa, tatizo lililopo ni mfumo mbaya wa utawala ndani ya CCM ambapo kila anayeingia atachafuliwa tu, hata Magufuli si safi labda atoke huko,” alisema.
Mratibu wa Chadema Kanda ya Magharibi, Christopher Nyamwanji alipongeza hatua ya kiongozi huyo kujiunga na chama hicho na kuwataka wana-Chadema wote kuwa kitu kimoja na kumpa ushirikiano wa hali ya juu na wenzake watakaohamia Ukawa.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Tabora Mjini, Saimon Lameck alisema wao hawana kinyongo na makada wanaohamia chama hicho kutoka vyama vingine, wanawakaribisha kwa mikono miwili.
Lowassa
Akizungumzia kujiondoa CCM jijini Dar es Salaam juzi, Lowassa alisema yaliyotokea Dodoma ameyatafakari na kwa mantiki hiyo atakuwa mnafiki kuendelea kubaki CCM.
Kuhusu Richmond Lowassa alisema yaliyotokea Dodoma, yamelitia dosari taifa na kwamba CCM aliyoiona Dodoma si ile ambayo amekulia kisiasa.
“Kama mtu aliye na uchungu na nchi yake nasema basi. Kama Nyerere (Julius) alivyosema CCM, si baba yake na si mama yake hivyo leo (juzi) nasema CCM si baba wala mama yangu, kama ni mabadiliko tutayapata nje ya CCM ambapo kuanzia leo (jana) nipo Chadema,” alisema Lowassa.
Pia, alisema alitangaza kugombea urais kupitia CCM mkoani Arusha pamoja na yaliyokea Dodoma bado safari yake ya matumaini ipo pale pale na kwamba alipewa hamasa na umati wa wananchi wakati akitafuta wadhamini mikoani kote

0 comments:

Post a Comment