Monday, 17 September 2018

KUMSALIA MAITI

Kumsalia maiti ni wajibu kwa Waislamu wote waliohudhuria na sio kwa mtu mmoja mmoja, kwa kiasi kwamba wakiitekeleza wanaotosheleza, walio baki wanakuwa hawana dhambi. Mtume, swallahlahu alayhi wasalam, amempa habari njema mwenye kumsalia maiti kwamba atapata malipo makubwa yanayolingana na mlima. Amesema: «Mwenye kuhudhuria Jeneza hadi akaswali, atapata Kirati, na mwenye kuhudhuria mpaka marehemu akazikwa atapata Kirati mbili. Mtume aliulizwa: Na Kirati mbili ni nini?  Alijibu: Ni mfano wa milima miwili mikubwa».  (Bukhari, Hadithi Na. 1325. Muslim, Hadithi Na. 945) .


Namna Ya kumswalia maiti


Namna yake ni kwamba maiti huwekwa mbele kati ya anayeswali na kati ya Kibla. Mwenye kuswali anasimama mbele ya kichwa cha mwanaume, na kwa mwanamke ansimama katikati yake, kama ilivyo nukuliwa kwa Mtume, swallahlahu alayhi wasalam. (Abudaud, Hadithi Na. 3196)


Inapendekezwa swala ya maiti ifanyike kwa Jamaa, na Imamu awe mbele ya maamuma, kama ilivyo kawaida katika swala ya Jamaa.


Mwenye kuswalia maiti ataleta Takbira nne kama ifuatavyo:


Takbira ya kwanza: Atasoma suratil Fatiha baada yake.




Takbira ya pili: Atamsalia Mtume baada yake kwa kutumia aina yoyote ya matamshi kama kusema:(Allaahumma Swalli wasallim Alaa Nabiyyinaa Muhammad = Ewe Mola wangu, mswalie na mdumishie amani Mtume wetu Muhammad. Kama atamswalia Mtume kikamilifu kama ambayo mwenye kuswali anasema katika Tashahudi ya Mwisho katika swala, inakuwa jambo kamilifu zaidi. Namna ya kumswalia Mtume kikamilifu ni hivi: (Allaahumma Swalli Alaa Muhammad. Wa Alaa Aaali Muhammad. Kamaa Swallaita Alaa Ibraahiim Wa Alaa Aali Ibraahiim. Innaka Hamiidun Majiid. Wabaarik Alaa Muhammad Wa Alaa Aali Muhammad. Kamaa Baarakta Alaa Ibraahiim Wa Alaa Aali Ibraahiim. Innaka Hamiidun Majiid = Ewe Mola wangu, mfikishie rehema Muhammad na familia ya Muhammad, kama ulivyomfikishia rehema Ibrahim na familia ya Ibrahim. Kwa yakini, wewe ni mwenye kusifika, mtukufu. Ewe Mola wangu, mbariki Muhammad na familia ya Muhammad, kama ulivyo mbariki Ibrahim na familia ya Ibrahim. Kwa yakini, wewe ni mwenye kusifika, mtukufu).


Takbira ya tatu: Baada yake atamuombea maiti rehema, msamaha, pepo na kunyanyuliwa daraja kwa yale ambayo Allah atayafungua katika ulimi wake na moyo wake. Kama mwenye kuswali anahifadhi baadhi ya dua zilizopokewa kwa Mtume kuhusu swala ya maiti itakuwa bora zaidi kuomba kwa kutumia dua hizo. Miongoni mwa dua hizo ni hizi zifuatazo: «Allaahummagh-firlahuu Warhamhu. Wa-aafihii Wa’fu Anhu. Wa-akrim Nuzulahuu. Wawassi’mudkhalahuu. Wagh-silhu Bilmaa’i wath-thalji Walbaradi. Wanaq-qihii minal-khatwaayaa Kamaa yunaq-qath-thaubul-abyadhwu Minad-danas. Wa-abdilhu Daaran Khairan Min-daarihii. Wa-ahlan Khairan Min-ahlihii. Wazaujan Khairan Min-zaujihii. Wa-ad-khilhul-jannah. Wa-aidh-hu Min-adhaabil-qabri au min-adhaabin-naar» (Ewe Mola wangu,  msamehe na mrehemu. Na muepushie mabaya  na msamehe. Na ukirimu ujio wake, na mpanulie makao yake na muoshe kwa maji na theluji na barafu na msafishe asiwe na madhambi kama nguo nyeupe inavyo safishwa ikawa haina uchafu. Na mbadilishie nyumba bora zaidi kuliko nyumba yake, na familia bora zaidi kuliko familia yake, na mke bora zaidi kuliko mkewe, na muingize peponi, na mkinge asipate adhabu ya kaburini au adhabu ya motoni.) (Muslim, Hadithi Na. 963)


Takbira ya nne: Baada yake atakaa kimya kidogo, kisha atatoa salamu upande wake wa kulia na wa kushoto, au upande wake wa kulia. Yote hayo yamethibiti kunukuliwa kwa Mtume, swallahlahu alayhi wasalam.


Sehemu ya kuswalia swala ya jeneza


Swala ya Jeneza inafaa kuswaliwa msikitini, au katika sehemu maalumu iliyoandaliwa nje ya msikiti kwa ajili hiyo, na pia inafaa kuswaliwa makaburini. Yote hayo yamethibiti kupokewa kwa Mtume, swallahlahu alayhi wasalam.




Mtume ametoa habari njema kwamba mazishi yana malipo makubwa.  

0 comments:

Post a Comment